F Ukweli kuhusu vyakula vya Wanga (kabohaidreti) | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Ukweli kuhusu vyakula vya Wanga (kabohaidreti)

Kabohaidreti ni kundi mojawapo kati ya makundi 6 muhimu ya vyakula. Vyakula vya kabohaidreti vimegawanyika kwenye makundi makuu matatu – wanga (starch), sukari (sugar) na ufumwele (nyuzinyuzi au fiber). Mwili hutumia zaidi kabohaidreti, wanga na sukari, kama chanzo kikuu cha nishati. Kabohaidreti inayozidi mwilini hubadilishwa na kuwa mafuta ili kuhifadhiwa kwa matumizi ya baadae.

Wanga
Vyakula vya kundi la wanga ni muhimu kwa mwili sababu ndio hasa chanzo kikubwa cha nishati mwilini.  Asilimia 60% hadi 70% ya kalori mwilini hutoka kwenye vyakula vya wanga. Ni vyakula vinavyotakiwa kuliwa kwa wingi ili kuweza kuufanya mwili kuendelea na shughuli zake kwa ufasaha.

Uzuri ni kuwa, vyakula vingi vyenye wanga huwa pia na virutubisho tofauti. Hii huufanya mwili kupata virutubisho vingi muhimu toka kwenye chakula moja. Mchanganyiko wa virutubisho pia hupunguza kasi ya unyonywaji wa sukari na vile virutubisho vinavyoweza kudhuru mwili.

Mfano wa vyakula vya wanga ni kama nafaka – mahindi, mchele, mtama.
Pendelea zaidi vyakula vyenye virutubisho mchanganyiko. Uwepo wa virutubisho mchanganyiko husaidia kupunguza madhara ya kirutubisho kimoja mwilini. Mfano, vyakula vyenye ufumwele hupunguza kiwango cha sukari kinachonyonywa kwenye damu na kukufanya uwe salama kwa muda mrefu.

Sukari
Sukari ni kundi muhimu sana la vyakula. Kwa ufupi, sukari ni muhimu ili kukuwezesha uendelee kuishi vizuri na mwili wako kufanya kazi vizuri. Vyakula vyote vya kabohaidreti husagwa ili kupata sukari aina ya glucose ambayo hutumika kwenye seli za mwili kama chanzo cha nishati. Glucose hutumika kwenye seli za mwili ili kuzipa uwezo wa kuendelea na kazi zake za kawaida.

Ni muhimu kuzingatia kuwa, sukari ni muhimu kwa mwili, lakini sukari inayoliwa kwa wingi kuzidi mahitaji ya wili huwa na madhara zaidi kuliko faida.

Fahamu kuwa kila chakula kina kiwango cha sukari, lakini kila aina ya sukari ina kiwango chake cha ufyonzwaji kwenye damu. Sukari nyingi huchukua muda kusagwa hadi kufikia glucose na kuingia kwenye damu. Mara nyingi vyakula vilivyo na mchanganyiko wa virutubisho tofauti huwa na hii tambia, na ndio vizuri kwa afya.

Glycemix Index (GI) ni kasi ya chakula katika kumeng’enya, kunyonywa sukari na kusababisha ongezeko la kiwango cha sukari kwenye damu. Vyakula vyenye glycemix index kubwa hunyonywa kwa kasi zaidi kuliko vile vyenye Glycemix Index ndogo. Kati ya vyakula vinavyosaidia kupunguza kasi ya unyonywaji wa sukari mwilini ni ufumwele (fiber).

Sukari ina madhara makubwa zaidi kwa mtoto anayekua, maana madhara ya ubongo atakayopata yanaweza kutorekebishika maishani mwake. Hivyo ni vizuri kumuepusha mtoto na sukari iliyozidi kiasi.

Haya ni baadhi ya madhara tofauti ya sukari:

  1. Kudhoofisha kinga ya mwili
  2. Kupunguza uwezo wa ubongo kufikiri kwa muda mrefu na umakini (short attention span)
  3. Sukari husababisha fetma (obesity)
  4. Kusababisha matatizo ya kongosho (pancreas) hivyo kupelekea ugonjwa wa kisukari.

Ufumwele
Virutubisho vya ufumwele, ambavyo hupatikana zaidi kwenye mimea, haviwezi kumeng’enywa mwilini, lakini vina faida muhimu kwenye kuboresha afya. Kati ya faida chache ni kusaidia kusafisha utumbo na kupunguza kasi ya unyonywaji wa virutubisho mwilini, hivyo kukufanya ujihisi umeshiba muda mrefu zaidi.

Kula vyakula vyenye ufumwele uweze kujisikia umeshiba kwa muda mrefu zaidi. Ufumwele hausagwi wala kunyonywa na mwili, hivyo husaidia kuboresha mfumo wa chakula na kusafisha matumbo.

Vyakula vya ufumwele vina faida tofauti mwilini, kati yake ni:

  1. Kupunguza kasi ya unyonywaji wa vyakula mwilini
  2. Kusafisha matumbo
  3. Kulainisha kinyesi
  4. Kuondoa uchafu na kemikali za sumu
  5.  Husaidia kupunguza unene wa mwili

Vyanzo vya kabohaidreti
Virutubisho vya kabohaidreti hupatikana kwa urahisi na kwa wingi zaidi kwenye nafaka, mfano mahindi, mchele, unga wa ngano. Vilevile, kabohaidreti hupatikana kwenye mizizi ya vyakula, mfano viazi, mihogo, magimbi.

Mahitaji ya kabohaidreti
Mahitaji  ya kabohaidreti hutofautiana kutokana na umri, jinsia, shughuli na hali ya kiafya.