Kwa njia moja au nyingine, unajikuta tumbo limechafuka kwa kujaa gesi, kuuma na hata kuunguruma, unahisi unahitaji kunywa dawa ili litulie.
Katika makala ya leo utajifunza njia bora ya kutuliza mchafuko wa tumbo kwa kutumia vyakula badala ya dawa za kisasa ambazo hutuliza dalili na haziondoi tatizo.
CHANZO
Kabla ya kukimbilia kwenye tiba ni vizuri kwanza kujua chanzo cha tatizo na katika hili unahitaji kujua ni vyakula gani ukila vinasababisha matatizo ya tumbo. Aina ya vyakula inaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu lakini kuna aina ya vyakula vinajulikana zaidi kusababisha matatizo ya tumbo.
Vyakula na vinywaji vinavyochangia tumbo kujaa na ukosefu wa choo kwa muda mrefu huwa ni soda, ulevi (hasa bia), vyakula vyenye mafuta mengi na vyenye chumvi nyingi.
Vyakula hivyo vinapoingia tumboni, huwa na tabia ya kuchelewesha usagaji wa chakula na uondoaji wa uchafu kwenye utumbo, hivyo huwa kikwazo katika mfumo mzima wa usagaji chakula kwa urahisi.
Ili kujiepusha na matizo ya tumbo ya muda mrefu na hata kuzuia uwezekano wa kuumwa na tumbo mara kwa mara, unashauriwa kula vifuatavyo, karibu kila siku ili kulifanya tumbo lako kuwa safi wakati wote:
PAPAI (PAPAYA)
Baadhi ya utafiti uliyopo, unaonesha kwamba ‘enzyme’ waliyomo kwenye papai husaidia usagaji wa chakula tumboni hivyo kulifanya tunda hili kuitwa na mtafiti wa zama za kale Christopher Columbus kama ‘tunda la malaika’.
Watafiti wamebaini kuwa tunda hili, lenye ladha tamu na harufu nzuri, huboresha mfumo wa usagaji chakula, husafisha utumbo, huzuia magonjwa ya uvimbe tumboni na huimarisha mfumo wa kinga ya mwili.
“Vitamini na virutubisho vya papai vina faida nyingi, lakini faida kubwa ya papai ipo kwenye kirutubisho (Enzyme) aina ya ‘Papain’ ambacho hujulikana kwa uwezo mkubwa ilionao wa usagaji mzuri wa chakula tumboni,” anasema Dk. Cari Case mwandishi wa blogu ya masuala ya afya.
Mwandishi huyo anaongeza kwa kusema kuwa papai limekuwa likitumika kama tiba tangu karne ya 18, lakini utafiti wa kisayansi haukugundua faida za papai hadi mwaka 1870 wanasayansi walipogundua kirutubisho cha papain kilichomo kwenye papai na tangu wakati huo tafiti nyingi zimekuwa zikifanywa kuhusu faida za tunda hili na uwezo wa tiba iliyonalo.
MTINDI (YOGURT)
Hata kama wewe si mpenzi wa mtindi, jaribu kunywa na utaupenda, hasa uwezo wake wa kuondoa matatizo ya kujaa gesi tumboni pamoja na matatizo mengine. Mtindi mzuri ni ule ‘plain’ ambao haujachanganywa na ladha au vitu vingine kwa lengo la kuongeza ladha. Bakteria asilia waliyomo kwenye maziwa mtindi ndiyo hufanya usagaji wa chakula kuwa mwepesi.
Mwisho, ili kupata faida ya papai na mtindi kama ilivyoelezwa hapo juu, ni vizuri ukala mara kwa mara kama siyo kila siku, kabla au mara baada ya kula vyakula ambavyo vinaweza kukuletea shida tumboni, au ukaweka mazoea ya kula kila siku ili kuliweka tumbo lako katika hali salama.