Alfajiri ya Jumamosi, 30 Desemba 2006 muda mfupi kabla ya saa 12:00, itakuwa siku ya kukumbukwa katika historia ya taifa la Iraq, kwa machungu au kwa furaha miongoni mwa wananchi wa taifa hilo kutokana na kunyongwa kwa aliyekuwa mtawala wa taifa hilo aliyeondolewa madarakani na majeshi ya kimataifa yakiongozwa na Marekani na Uingereza.
Saddam Hussein Abd al-Majid al-Tikriti, ambaye alikuwa mtawala wa taifa la Iraq amekabiliwa na changamoto ya msemo huo kufuatia kutekelezwa kwa hukumu iliyotolewa na mahakama moja nchini Iraq ya ‘kunyongwa hadi kufa’ baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa kibinadamu uliomkabili licha ya kukata rufaa na ktupwa baadaye.
Wengi tulizoea kusikia majina yake ya Saddam Hussein, lakini majina yake halisi ni kama yalivyotajwa hapo juu na alizaliwa tarehe 28, Aprili mwaka 1937 katika kijiji cha Tikrit katikati ya Iraq, na aliingia madarakani tarehe 16 Julai 1979 na kulitawala taifa hilo kwa mkono wa chuma hadi tarehe 9 Aprili 2003 alipoondolewa kwa nguvu na majeshi hayo.
Hukumu hiyo ambayo inatia simanzi na furaha kwa pamoja kulingana na mitazamo ya watu kuhusiana na sakata la kuibuka na kuporomoka kwa Saddam imetekelezwa kwa wakati kama alivyoahidi Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Nouri al-Malik, kwamba hukumu dhidi ya kiongozi huyo itatekelezwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Kuuawa au kunyongwa kwa Saddam imekuja kufuatia hukumu iliyotolewa na Mahakama Maalum iliyomtia hatiani kwa mauaji ya wanakijiji waarabu wa madhehebu ya Shia wapatao 150 baada ya kushindwa kwa jaribio la kumuua mwaka 1982.
Pia akikabiliwa na mashitaka mengine ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wakurdi 180,000 wengi wao wakiwa raia wa Iraq mwishoni mwa miaka ya 1980.
Kiongozi huyo aliyeitawala Iraq kama rais wa tano wa nchi hiyo alionekana akiwa na amebeba kitabu kitukufu cha Koran huku akisema kwa sauti kuu kuwa 'hakuna Mungu mwingine bali Allah na Muhammad ni Mtume wake', alinyongwa katika kasri ya wizara ya Sheria.
Kufuatia kifo hicho habari zinaeleza kuwa katika jiji la Washia la Sadr karibu na Baghdad, watu wameonekana wakicheza na kushangilia mwisho wa maisha ya Saddam, huku kusini mwa jiji la Baghdad mlipuko wa bomu umewaua watu wapatao 30 katika soko la samaki.
Mwezi Oktoba, 1959 alihusika katika jaribio lililoshindikana la kumuua mtawala wa Iraq kipindi hicho, Jenerali Abdul Karim Qassem, na kukimbilia uhamishoni katika nchi ya Misri alikoishi kwa miaka minne.
Saddam alirejea Baghdad Februari, 1963 na kujiunga na chama cha Baath kilichoingia madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na kuondolewa madarakani miezi tisa baadaye, na viongozi wa chama hicho kutupwa gerezani.
Hata hivyo alichaguliwa kuwa Makamu Katibu Mkuu wa chama hicho akiwa gerezani huku wenzake wakiendeleza harakati za mapinduzi ambayo yalifanikiwa miaka mitano baadaye.
Akiwa mwanachama na kiongozi wa chama cha Baath Arab Social Party kilichofuata sera za ujamaa wa kiarabu na uchumi ulioendelea, Saddam alichukua jukumu kubwa la kuhakikisha kwamba anastawisha maisha ya wananchi wake huku akikazana kuleta mapinduzi ya kiuchumi miongoni mwa mataifa yaliyoko kwenye jumuiya ya kiarabu.
Saddam ambaye ameacha wajane watatu; Sajida Talfah, Nidal al-Hamdani na Samira Shahbandar alikuwa miongoni mwa viongozi wa mstari wa mbele katika mapinduzi yaliyokiweka chama chake madarakani Julai 1968 baada ya kumuondoa madarakani, Abdul Mohamed Aref, na kukiwezesha kutawala Iraq kwa kipindi kirefu.
Akiwa Makamu wa Rais chini ya uongozi wa mpwa wake, Jenerali Ahmed Hassan al-Bakr, Saddam aliongoza na kuendekeza chokochoko baina ya utawala na viongozi wa kijeshi katika utawala huo na kuimarisha wapambe wake katika safu ya uongozi na usalama kwenye kada ya utawala kwa lengo la kudhoofisha uongozi wa kijeshi.
Wakati rais wa nne wa Iraq, Jenerali Hassan al-Bark akijihusisha na kazi ya kutaifisha kampuni kubwa ya uchimbaji mafuta ya Iraq Petroleum Company na kuyalipa makampuni mengine ya kigeni na kuyaondoa nchini, Saddam alikuwa akijikita katika kufanya kazi ya kuhakikisha kuwa anaendelea kujijenga katika uongozi wa Iraq.
Utawala wa Baath ulikabiliwa na upinzani kutoka kwa Wakurdi ambao waliendeleza chokochoko dhidi ya utawala wa Baghdad na kupelekea kusainiwa kwa kwa mkataba wa mpaka baina ya Iraq na kiongozi wa kidini wa Iran, Shah mwezi Machi 1975; ingawaje Shah huyo aligeuka na kuendelea kuwapa misaada wakurdi hao.
Kiongozi wa Iraq, Jenerali Hassan al-Bark, alilazimika kustaafu kwa kilichoelezwa kuwa na umri mkubwa mwezi Julai 1979 na Saddam ambaye alikuwa muislamu wa madhehebu ya Sunni alichukua uongozi wa taifa hilo ingawaje wadadisi wa mambo ya kisiasa wanadai kuwa Jenerali huyo alilazimika kustaafu kufuatia saddam kujiimarisha na kuchukua uongozi usio rasmi wa taifa.
Ghasia zilizoendelezwa na Wakurdi katika mpaka wa Iran na Iraq ilipelekea kuanza kwa vita vilivyodumu kwa miaka minane kati ya Iran na Iraq, mwezi Septemba 1980.
Iraq ambayo imetokea kuwa wahasimu wakubwa wa Marekani, katika vita hivyo ilikuwa ikisaidiwa na taifa hilo kubwa duniani dhidi ya Iran katika vita vilivyogharimu maisha ya watu wapatao milioni moja .
Alipigana vita hivi kwa lengo la kuondoa tishio la kikabila na kidini lililokuwa likiukabili utawala wake kutoka kwa makundi yaliyokuwa yakitaka kujitawala au kupewa uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe ndani ya mipaka ya kikabila na kidini nchini Iraq.
Wakati wa vita hivyo, Saddam alijulikana kama shujaa pekee wa Kisunni aliyesimama kidete dhidi ya wahasimu wa Marekani na Israel katika jumuiya ya kiarabu na hii ilimjengea heshima mbele ya mataifa hayo ambayo yalikuja kumgeuka baadaye kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa amani mwezi Agosti, 1988 kati yake na Iran.
Katika vita hivyo, kiongozi huyo wa Iraq alijivunia nguvu za maaskari wake 190,000, vifaru 4,500, magari ya kivita4,000, ndege za kivita 500 na helikopta 400 dhidi ya Iran ambayo ilikuwa na nguvu za wanajeshi 305,000, wanamgambo 500,000, vifaru 1,000, ndege za kivita 65 na helikopta720.
Ingawaje chaguzi kadhaa za urais zimeendeshwa kipindi cha utawala wake, Saddam aliwachukulia hatua kali na za mateso watu wote walionyesha kuupinga utawala wake, waliokataa kupiga kura au waliopiga kura za kumpinga.
Urafiki wa iraq na Marekani uliingia nyongo pale alipojaribu kutikisa nguvu za taifa hilo kwa kuivamia nchi ya Kuwait mwezi Agosti 1990 na kupelekea Marekani kuendesha vita vilivyojulikana kama 'Operation Desert Storm' dhidi ya uvamizi huo.
Katika kuuonyesha ulimwengu kuwa ana nguvu katika nchi yake, Saddam aliitisha uchaguzi nchini humo na kubuka kidedea kwa kupata zaidi ya asilimia 99 za kura zote na Oktoba mwaka 2002 akajinyakulia asilimia 100 za kura katika uchaguzi mwingine wa urais nchini Iraq.
Baada ya kujijengea uadui na Marekani na mshirika wake Israel, Marekani iliendeleza chokochoko dhidi ya utawala wa Iraq ikidai kuwa nchi hiyo ina akiba kubwa za kemikali na silaha za nyuklia na hivyo kuihusisha na kundi la magaidi la al-Qaeda la Osama bin Laden.
Madai hayo hata hivyo yalikanushwa vikali na Saddam mwezi Februari, 2003 lakini ilipofika tarehe 20 mwezi Machi 2003, Muungano wa mataifa kadhaa ukiongozwa na Marekani uliivamia Iraq kinyume cha azimio la Umoja wa kimataifa (UNO) lililokataa kuchukuliwa kwa hatua hiyo.
Aprili 9, 2003 majeshi ya marekani yalifika katika jiji la Baghdad na kuwaua watoto wa Saddam; Uday na Qusay Hussein baada ya kushambulia makazi yao kwenye mji wa Mosul Julai 22.
Mtawala huyo alikwenda mafichoni kuepuka kukamatwa na majeshi ya Marekani na washirika wake lakini juhudi za kukwepa mkono wa majeshi hayo hazikuzaa matunda kwani ilipofika tarehe 13 desemba 2003 alitiwa mbaroni na kukamatwa kwake kukatangazwa rasmi.
Tarehe 19 Oktoba 2005, Saddam alifikishwa mbele ya mahakama maalum kusikiliza mashitaka ya mauaji ya 1982 ya washia 150 katika mji wa Dujal baada ya jaribio lao la kumpindua kushindikana na Agosti 21, 2006 mahakama ikaanza kusikiliza mashitaka mengine ya mauaji ya maelfu ya Wakurdi 1988.
Majaji wa mahakama hiyo waliteuliwa na Baraza linalotawala nchini Iraq kwa kushauriana na Baraza la Sheria na kupewa kazi kwa miaka mitano likiongozwa na Jaji Rizgar Mohamed Amin akisaidiwa na Rauf RashidAbd al-Rahman na wengine.
Mahakama hiyo ilimkuta saddam na hatia ya makosa dhidi ya Ubinadamu tarehe 5 septemba 2006 na kumhukumu kunyongwa, hukumu ambayo aliikatia rufaa ingawaje Mahakama Kuu ya Rufani ya Iraq iliitupilia mbali rufani yake 26 Desemba 2006 na kushikilia hukumu ya kunyongwa, zoezi ambalo limetekelezwa na kuhitimisha historia ya Saddam Hussein.