F Jenista Mhagama azungumzia ajira nje ya nchi | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Jenista Mhagama azungumzia ajira nje ya nchi


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amesema kupitia utafiti uliofanywa na tume yake wamegundua fursa nyingi za kazi kwa vijana wa kitanzania zinazopatikana katika mataifa ya kiarabu.

Waziri Mhagama ametoa kauli hiyo leo Bungeni  (Aprili 06, 2018) kwenye mkutano wa 11 unaoendelea kufanyika mkoani Dodoma wakati akitoa ufafanuzi juu matatizo mbalimbali wanayokumbana nayo raia wa kitanzania pindi wanapotafutiwa kazi na mawakala katika nchi za nje ambapo kwa kipindi kirefu kumekuwepo na malalamiko mengi kutokana na unyanyasaji wanaoupata.

"Kwa kipindi kirefu tumekuwa tunapokea malalamiko ya watanzania na baadhi ya wafanyakazi wengine kutoka mataifa ya Afrika wanavyopata shida wanapokwenda kufanya kazi nje ya nchi zao. Huduma hii ya kuwaunganisha watanzania na watafuta kazi nje ya Tanzania nilisimamisha huduma hii hapa katikati ili niweze kufanya ukaguzi wa kutosha na kujiridhisha kama mawakala hao wanafanya kazi kwa kufuata sheria...

Tumegundua kwamba zipo fursa nyingi za ajira nje ya nchi yetu ya Tanzania kama vile Saudi Arabia, Qatar na nchi nyingine, lakini aina ya ujuzi unaotakiwa kule nje na kama tutajipanga vizuri serikali na kuanza kufanya hivyo tuna uwezo wa kuwapeleka watanzania wengi kwa mikataba rasmi na wakarudisha mapato ya kutosha katika nchi yetu", amesema Mhagama.

Pamoja na hayo, Waziri Mhagama ameendelea kwa kusema "kule Saudi Arabia wanahitaji wafanyakazi zaidi ya elfu mbili wa ujuzi wa kati na juu kwenye fani kama urubani, madaktari, ualimu na madereva, nina lihakikishia Bunge baada ya ripoti hii tutaweza kujipanga sawa sawa na watanzania wataweza kupata ajira zenye staha nje ya nchi na kurudisha mapato nchi".

Kwa upande wake, Naibu waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika ya Masharika Dkt.Suzan Kolimba amesema serikali itaendelea kuwadhibiti mawakala wanaoshughulika na kuwatafutia watanzania ajira nje ya nchi ili kuwafanya waajiriwa hao wawe salama.