Maswala ya uzazi na malezi kwa wanawake ni jambo lililo wazi kabisa lakini kutokana na maadili baadhi wamekuwa na woga wa kujadili wazi wazi. Hata vivyo baadhi ya wanawake hawa hupenda kuzungumzia maswala haya hasa wanapo kutana ili kubadilisha mawazo na hata kujifunza zaidi.
Uwepo wa mitandao ya kijamii umesaidia sana katika kuwakutanisha wanawake kutoka maeneo mbali mbali ambapo hujadili zaidi maswala ya mahusiano uzazi na uchumi au naweza sema fursa za kibiashara.
Katika swala la uzazi majadiliano mara kwa mara yamekuwa ni kuhusu malezi, kunyonyesha kipindi cha mimba na hasa njia gani itumike katika uzazi wa mpango ambayo ni salama na haina madhara.
Kuna ambao hutumia njia za asili za uzazi wa mpango, mfano mbinu ya kutegemea kalenda ambayo hufuata mzunguko wa hedhi au kumwaga mbegu za kiume nje ya njia ya uzazi.
Baadhi ya wanawake huchagua kutumia njia za uzazi wa mpango za kisasa, mfano: kuweka kitanzi au sindano.
NJIA MBALI MBALI ZA KISASA ZA UZAZI WA MPANGO
•Njia ya Vidonge
•Njia ya sindano
•Kutumia kizuizi yaani kondom ya kike au ya kiume
•Kuweka Kitanzi
•Kuweka kipandikizi/ Kijiti
Hata hivyo kumekuwa na majadiliano ama jumbe mbali mbali katika mitandao ja kijamii zinazo zungumzia madhara ya njia za kisasa za uzazi wa mpango.
Baadhi ya madhara yanayo tajwa na wanawake katika jumbe mbali mbali pamoja na mitandao ya kijamii ni pamoja na kupata ugumu wa kushika mimba baada ya kutumia njia hizo, kutokwa na damu mara kwa mara, kupungua au kuongezeka mwili, kuongezeka kwa hamu ya kula, kupotea kwa hamu ya tendo la ndoa, mabadiliko ya siku za hedhi, maumivu ya kichwa, nk.
BBC imefanya mazungumzo na baadhi ya wanawake juu ya uzoefu walio nao kuhusu matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango na kufahamu je ni kweli baadhi yao hupata madhara tajwa.
"Mimi nimewahi kutumia njia ya uzazi wa mpango ya kuweka kijiti, nimetumia kwa takribani miaka miwili. Iliwahi kuniletea matatizo, ule mwaka wa kwanza nilienda vizuri ila mwaka wapili iliniletea shida nilikua naingia hedhi baada ya wiki moja inatoka unakaa kidogo inatoka tena yaanini nilikuwa natokawa na damu hovyo hovyo tu na sio kwamba ilikuwa inatoka kwa mpanginio nivitone vitone tu, kwakweli saivi natumia kalenda," anasema Mkwama mama wa watoto watatu.
"Mi nilikuwa nataka kupangilia watoto wangu nikatumia njia ya kijiti,kwamara ya kwanza kilini faa tu lakini nilipo pata mimba ya pili nikaamua kutumia tena kijiti kikanikataa yaani nikawa kila baada ya wiki mbili naingia kwenye hedhi kwa hivo ndipo niliamua kukitoa. Kwa sasa natumia kalenda tu," Agness Tamam anaiambia BBC.
Baadhi wanasema unapoweka njia hizi unapata dalili zote za mtu mwenye mimba.
"Mie nlikuwa kama nina mimba kwa ile miezi miwili yakwanza nlipoweka Kitanzi, maziwa yalituna , kichefu chefu na kizunguzungu ila baada ya muda nikawa sawa na ninacho mpaka sasa," Rehema anaiambia BBC.
BBC imefanya mazungumzo na Sista Selesina Chambo afisa muuguzi mwandamizi wa Hospitali ya Taifa ya muhimbili ambaye pia ni mtaalamu wa maswala ya uzazi wa mpango.
"Kuna makundi ya njia za uzazi wampango, zenye vichocheo na zisizo na vichocheo. Zile za kundi la kwanza zisizo na vichocheo kama lupu na kondomu mara nyingi hakuna na mabadiliko, hakuna ongezeko la kutoka kwa damu wala kichefu chefu. Hizi za kundi la pili zilizobeba vichocheo, zinakuwa na maudhi madogo madogo kama vile kuongezeka kwa wingi wakati wa hedhi au baada ya kutumia mfano sindano,mtu anaweza akahitaji ujauzito alioupanga akakaa kwa muda mrefu bila kupata. Kuna kero zingine kama kuongezeka uzito na kupata kichefu chefu lakini haya yanatokea miezi mitatu ya mwanzo pekee baada ya hapo yanatoweka," Chambo anaiambia BBC
Hata hivyo mtaalamu huyo akatoa ushauri kwa wanawake na wanaume kuwa ni vyema wakazielewa njia zote za uzazi wampango kabla ya kutumia.
"Ili upate huduma sahii anapohitaji kuanza uzazi wa mpango aende kwa mtoa huduma sahihi ambaye amesomea njia zote za uzazi wa mpango, ili kabla ya kupewa afanyiwe ushauri wa kina aelewe kitakacho tokea, na hatuiti madhara tunaita maudhi madogo madogo" anasisitiza Chambo.
Hata hivyo ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu matumizi ya njia za uzazi wa mpango imeonyesha ongezeko katika baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania. Takwimu zinasema kuwa matumizi sasa ni asilimia 27 ya watanzania wenye uwezo wa kutumia njia hizo ikiwemo sindano, vipandikizi na mipira ya kiume na ya kike.
Mada zinazohusiana