F Muhimbili yaanza kutibu Wagonjwa wenye uvimbe | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Muhimbili yaanza kutibu Wagonjwa wenye uvimbe


Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), imeanza kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa uvimbe sehemu za kinywa, usoni na shingoni ambayo ilikuwa ikipatikana nje ya nchi.

Kuanza kutolewa kwa matibabu hayo nchini, kumewezesha kuokoa Sh. milioni 96 alizokuwa akilipa mgonjwa mmoja kutibiwa nje ya nchi, lakini nchini inatolewa kwa Shilingi milioni nane kwa mgonjwa.

Akitangaza kuanza kwa huduma hiyo nchini, Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi wa MNH, Dk. Praxeda Ogweyo, alisema huduma hiyo ilianza mwaka jana na tayari wagonjwa 45 wameshapatiwa matibabu.

Alisema matibabu ya magonjwa hayo ya aina mbili ni 'Haemangioma' ambao ni wa kuota uvimbe sehemu za kinywa kama kwenye ulimi, usoni na shingoni, ambao dalili zake ni mtoto kuzaliwa na alama nyekundu katika maeneo ya mwili wake.

Mwingine ni 'Iymphangioma' ambao ni uvimbe unaoanza kuota kama kipele katika sehemu za mwili ambacho si saratani na husababishwa na kukua au kuvimba kusiko kawaida kwa mishipa mikubwa ya damu.

Dk. Ogweyo, alisema magonjwa hayo yanawapata zaidi wanawake, watoto wa kike na wasichana kwa asilimia 70, huku wanaume wakipata kwa asilimia 30 ingawa bado hawajafahamu sababu.

Pia alisema matibabu yake yanatolewa kwa awamu nne, ili mgonjwa arejee katika hali yake ya kawaida.

“Jumla ya wagonjwa 45 wamenufaika kwa gharama ya Sh. milioni 360 sawa na Shilingi milioni nane kwa kila mgonjwa. Kama wangeenda nje ya nchi ingeigharimu serikali Sh. bilioni 4.320, sawa na Sh. milioni 96 kwa kila mgonjwa," alisema na kuongeza:

“Hospitali ya Muhimbili imeokoa kiasi cha Sh. bilioni 3.96 kwa kutoa huduma hiyo hapa nchini. Uwepo wa huduma hii nchini utasaidia wananchi wengi kunufaika na hatimaye kupunguza mzigo wa kulipa fedha nyingi kwa matibabu huko nje ambao nchi ya India ndiyo inatoa huduma hii."

Naye Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Kinywa, Meno na Uso, Dk. William Sianga, alisema wanatoa matibabu kwa kutumia vifaa vya radiolojia kama X-Ray, MRI, CT-Scan na Ultra-Sound kutibu moja kwa moja ugonjwa au kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi.

Alisema pia wanatibu kuondoa uvimbe kwenye sehemu ya kinywa, uso na shingoni, kuweka mirija kwenye figo ambazo mirija ya kutoa mkojo imeziba, kuzibua mirija ya nyongo iliyoziba, kuzibua mirija ya uzazi iliyoziba na kunyonya usaha ndani ya tumbo.