F Serikali yashauriwa kutatua changamoto hasa masuala ya udhalilishaji wa Wanawake | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Serikali yashauriwa kutatua changamoto hasa masuala ya udhalilishaji wa Wanawake


Na Thabit Hamidu,Zanzibar.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) imeshauriwa kuangalia namna ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kisiwani Tumbatu hasa masuala ya udhalilishaji wa wanawake na watoto pamoja na kutelekeza Familia unaofanywa na kina baba kisiwani humo

Hayo yamebainishwa na Wanaharakati wa kutetea haki za wananwake na watoto kutoka Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA wakati wa kikao cha Kutathimini mradi wa malezi mbadala Unaotekelezwa na kisiwani tumbatu chini ya ufadhili wa kijiji cha Malezi  S.O.S  na  Tamwa.

Ambapo fedha za kuendeshea mradi huo zimetoka kwa washirika wa maendeleo chini Dermark.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Tamwa Zanzibar Mratibu wa Mradi huo Mariam Ame  alisema licha ya jitihada zinazochukuliwa na Serikali pamoja na Asasi za kiraia lakini bado kumeonekana kuwepo kwa mfumo dume unaosababisha watoto kukosa haki zao za msingi na kuonekana kwa malezi ya mapamoja jambo ambalo linapelekea viashiria vya hatari ya kukumbana na masuala ya udhalilishaji

Miongoni mwa mambo yaliyoibuliwa katika utekelezaji wa Mradi huo katika kisiwa cha Tumbatu ni kuendelea kwa maswala ya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto ambayo hadi sasa wakazi wa kisiwa hicho wamekuwa na muhali katika kuyaripoti matukio hayo.

Alisema kwa mujibu wa Katibu tawala wa wilaya Ndogo ya Tumbatu kuna kesi nyingi ambazo hazijaripotiwa kutokana na Tabia ya wananchi wengi kujadili na kusuluhishana wenyewe kwa wenyewe.

Alisema Tumbatu kunahitajika kutolewa elimu juu maswala ya udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ikiwemo jamii hiyo kujua athari zinazotokana na vitendo vya udhalilishaji kwa watoto.

Aidha kwa Upande wake mratibu wa malezi mbadala kutoka katika Vijiji vya kulelea watoto yatima SOS Nyezuma Simai Issa alisema Mradi huo unalengo la kuwapa malezi bora kwa watoto ambao wamepoteza mzazi mmoja pamoja na familia ambazo zinaisha katika mazingira magumu.

Alisema Mradi huo ambao unatekeleza mambo matatu ikiwemo kuwajengea uwezo wadau kuhakikisha kwamba lengo la mradi la malezi mbadala linafanikiwa Miongoni mwa wadau hao ni asasi za kirai, masheha, pamoja na maafisa kutoka serikalini.

Aidha alisema mradi huo pia ulitenga fungu dogo katika kuboresha huduma za malezi ikiwemo elimu, Afya, na kuwapatia jamii mtaji ili kuendesha maisha yao na kulea familia zao.

Jumla ya familia 50 katika kisiwa cha Tumbatu zimefaidika na Mradi huo wa malezi mbaladala ikiwemo watoto wa kike 29 na wakiume 21 wakiwa chini ya walezi 31.

Mradi huo wa malezi mbadala unateekelezwa katika nchi 3 za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Rwanda, Tanzania/ Zanzibar na unaotekelezwa katika kijiji cha SOS Zanzibar kwa kushirikiana na asasi za kirai kama vile TAMWA, MUZDALIFA, na kufadhiliwa na SOS Denmark.