F Sheria ya kudhibiti mavazi ipo - Mwanasheria Mkuu Zanzibar | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Sheria ya kudhibiti mavazi ipo - Mwanasheria Mkuu Zanzibar


Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameambiwa kuwa Sheria ya Kudhibiti mavazi yanayofaa kutumiwa na Wazanzibari kwa ajili ya kulinda mila na utamaduni wao ipo.

Mwanasheria mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Said Hassan Said alisema hayo wakati akijibu hoja za wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliojadili bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliochangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria walitaka kujua kwa nini serikali haitaarishi sheria itakayodhibiti mavazi ya utamaduni wa kitaifa.

Said alisema sheria ya mavazi ya Zanzibar ipo tangu mwaka 1973 ambayo ni sheria No.1 ya mwaka 1973 na kujulikana sheria ya kulinda utamaduni wa kitaifa. Nimeiona sheria ya mavazi ya Zanzibar na nimeileta na kumkabidhi mwakilishi Panya(Ali Abdallah) kuisoma na kuipitia.Zanzibar inaongoza kuwa na sheria nyingi ingawa tatizo ni utekelezaji wake na usimamizi,"alisema.

Alisema sheria hiyo imeweka vizuri utaratibu na aina gani ya mavazi ambayo wananchi wanalazimika kuyatumia ikiwemo wanawake na wanaume.

Alifahamisha kwamba katika sheria hiyo hakuna mwanya na nafasi ya kuwepo kwa mavazi yanayokwenda kinyume na maadili na heshima ya binaadamu. Sheria kitu kimoja na utekelezaji wake jambo jingine, wazazi ndiyo wanaowanunuliya nguo za ajabu watoto na kuwashajihisha kuzitumia,"alisema.

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein akizungumza na uongozi wa Wizara ya Vijana na Utamaduni Ikulu ndogo Kibweni Unguja, alisisitiza suala la mavazi yatakayokwenda sambamba na utamaduni wa Mzanzibari.