Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amekitaka Chuo cha Ardhi cha Tabora kuandaa Mitaala ya elimu itakayoendana na changamoto ya soko la ajira kwa wahitimu wake.
Lukuvi alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki alipozungumza na Watumishi pamoja na Wanafunzi wa Chuo cha Ardhi Tabora alipokuwa katika ziara ya kuzindua Mpango Kabambe wa Uendelezaji Mji wa Tabora pamoja na Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika kijiji cha Sojo mkoani Tabora.
Alisema, 'ni vyema katika kipindi hiki ambacho kuna changamoto za ajira chuo hicho kikaenda mbali zaidi kwa kubuni kozi ambazo wanafunzi watakaohitimu katika chuo hicho watakuwa na uwezo wa kujiajiri badala ya kutegemea ajira ya serikali.'.
Kwa mujibu wa Lukuvi, kwa sasa ajira inayopatikana kwa wahitimu wa vyuo vya ardhi haizidi asilimia 10 jambo linalosababisha idadi kubwa ya wahitimu kuwa mtaani bila kuwa na ajira. "Hakuna namna mhitimu wa chuo cha ardhi akaenda mtaani na kujua maisha halisi ya sasa kwa kuwa na taaluma itakayojumuisha mambo tofauti yatakayomuwezesha kupambana na soko la ajira" alisema Lukuvi.
Waziri Lukuvi alitolea mfano kwa wanafunzi wanaosomea Kozi ya Kurasimu Ramani kuwa ingekuwa bora zaidi kwao wakaongezewa somo la Upimaji ili kuwa na taaluma pana itakayowawezesha kwenda sambamba na changamoto ya ajira iliyopo sasa.
Lukuvi aliongeza kuwa, sasa hivi Wizara ina kazi kubwa ya kurasimisha maeneo yasiyopimwa na furaha yake ni kuona wahitimu wa vyuo vya ardhi nchini wanashiriki kazi hiyo hata kwa kujiunga vikundi na kuanzisha kampuni itakayojishghulisha na kazi ya kupima na kupanga ambapo alisisitiza kuwa suala hilo litafanikiwa iwapo wahitimu wa vyuo vya ardhi watakuwa na taaluma mtambuka.