F Kilimo bora cha maboga | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Kilimo bora cha maboga

Boga ni zao ambalo mmea wake unakuwa kwa kutambaa na ni la mviringo, ngozi yake ni nyororo na rangi yake ni ya njano inayoelekea kwenye rangi ya chungwa au rangi ya kijani. Katikati ya boga kuna mbegu na massa, Boga lipo katika jamii ya Cucurbita pepo.

Asili yake
Asili ya boga ni Amerika kaskazini, maboga yamekuwa yakipandwa kwaajili ya biashara na kwaajili ya chakula. Kwa sasa maboga yamekuwa yakilimwa maeneo mbalimbali duniani, Antarctika pekee ndiko maboga hayawezi kustawi. Mataifa yanayozalisha maboga kwa wingi ni Marekani (USA), Canada, Mexico, India, and China.

Hali ya hewa & udongo 
Maboga yanahitaji joto la wastani kutoka kwenye jua, pia eneo ambalo halituamishi maji udongo wake uwe na pH kati ya 6.0 – 6.8. Pia udongo uwe na joto inchi tatu (sm 7.6) kushuka chini angalau nyuzi 60 °F (15.5 °C), maboga yatadhoofika kama maji yatakosekana.

Utayarishaji wa shamba
Shamba litayalishwe kwa umakini bila kuwa na sehemu ya kutuamisha maji maana mmea wa maboga na maboga yenyewe hutambaa chini, tumia jembe la ng’ombe, trekta, jembe la mkono au pawatila, changanyia mbolea za asili (samadi au mboji) na udongo ili kurutubisha shamba.

Utayarishaji wa mbegu
Mbegu za maboga zinatoka ndani ya maboga, kuna mbegu zilizoboreshwa (za kisasa) na za asili, andaa mbegu mapema wiki moja au mbili kabla ya kupanda.

Upandaji
Maboga hupandwa kwa kufukia mbegu sentimita 1 au 2 chini ya udongo , panda mbegu 2 kila shimo. Pia panda umbali wa sentimeta 30 kutoka shina hadi shina na mita 1.5 – 2 kutoka mstari hadi mstari.

Matandazo (mulches )
Kwasababu ni zao linalotambaa basi lazima tuangalie namna ya kutandaza, weka nyasi na mabaki ya mimea mingne kufunika ardhi. Baada ya miche kutambaaa kwa kiasi unaweza kuweka matandazo (mulches) ambayo yaweza kuwa nyasi kavu kwenye udongo ili kuzuia upotevu wa unyevu vile vile kupunguza uotaji wa magugu shambani kwako. Vile vile matandazo yakioza yanaongeza rutuba kwenye udongo na hulinda udongo dhidi ya mmomonyoko wa udongo.

Mbolea
Katika matumizi ya mbolea yanatofautiana kutokana na mbegu, Lakini tumia mbolea za asili (samadi au mboji) ili kuongeza rutuba kwenye udongo, ukihitaji kutumia mbolea za viwandani weka kiasi sana, labda eneo hilo kama hakuna rutuba, mbolea ya NPK inaweza tumia.

Upaliliaji & unyevu
Palilia shamba nyasi zinapoanza kuota, pia safisha shamba ili kuondoa wadudu. Shamba la maboga linatakiwa liwe na unyevunyevu kila mara ili maboga yaweze kustawi vizuri yasidumae.

Uvunaji
Maboga hukomaa baada ya siku 95 mpaka 120, ili kujua kuwa boga lako limekomaa unaangalia kikonyo, kikonyo cha boga kinapoteza maji na kinaanza kuwa kikavu.