F Halmashauri ya wilaya ya Njombe yapata eneo la kuhamia kwa dharula | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Halmashauri ya wilaya ya Njombe yapata eneo la kuhamia kwa dharula



Na  Amiri kilagalila-Njombe

Baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Njombe limekutana kwa dharula na kukubali mapendekezo ya wataalamu wa halmashauri hiyo,kuhamia kwa muda katika eneo la Mtwango lenye ekali zaidi ya 12 linalomilikiwa na halmashauri hiyo na kujenga mabanda ya muda ili kutii maelekezo ya Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli yaliyotolewa akiwa katika ziara yake Mkoani Rukwa.

Awali akitoa taarifa ya mapendekezo ya wataalamu,mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Ally Juma Ally,amesema kikao cha dharula cha wataalamu  kilibaini kutokuwepo kwa GN inayotambulisha eneo la makao makuu ya halmashauri,na kupendekeza kuhamia kwa haraka katika eneo la Mtwango kwa muda ili kutekekeleza agizo la Rais na kuepuka wimbi la kufutwa.

Aidha amesema miongoni mwa sababu za mapendekezo ya kuhamia katika eneo hilo ni pamoja na kupitiwa na mkonga wa Taifa wa mawasiliano,pamoja na uwepo wa nyumba za kujihifadhi watumishi kwa kipindi hiki cha dharula.

“Wataalamu wamependekeza kuhamia katika eneo hili kwasababu eneo hili limepitiwa na mkonga wa Taifa wa mawasiliano hivyo itakuwa ni rahisi kuhamisha miundombinu ya mawasiliano ya halmashauri,lakini pia eneo la Mtwango tuna eneo la ekari zaidi ya 12 linaloweza kujenga mabanda ya dharula na kuhakikisha tukahamia kwa kipindi hiki kifupi,lakini sababu nyingine ni uwepo wa huduma za jamii kwasababu tunawatumishi zaidi ya 100 tunaotakiwa kuhama na leo tumebakiwa na siku 26 ili kutii maelekezo na halmashauri yetu isiingie katika wimbi la kufutwa”alisema Ally Juma Ally.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Valentino Hongoli amewashukuru madiwani kwa kulidhia uhamisho huo na kumtaka mkurugenzi kuanza maandalizi na kuhamia katika maeneo hayo.

“Ninawashukuru madiwani kwa utayari huu na nina amini maamuzi haya yatamuwezesha mkurugenzi wetu mara moja kuanza kwenda kufanya maandalizi pamoja na kuhamia kwasabau siku tulizo pewa ni 30 kwa hiyo bado siku 26 tu”alisema Hongoli.


Madiwani wa halmashauri wameshukuru kwa ufafanuzi uliotolewa na mkurugenzi,na kuahidi kutekeleza agizo la Rais bila kuathiri shughuli za halmashauri hiyo.

Jumla ya halmashauri 31 nchini, ambazo ofisi zao zipo nje ya maeneo yao ya utawala ikiwemo halmashauri ya wilaya ya Njombe zimeagizwa kuhamishia ofisi hizo katika maeneo yao ya utawala ndani ya siku 30 huku halmashauri itakayochelewa kutekeleza agizo hilo kufutwa.