F Waziri Ummy Mwalimu awataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuacha kuendekeza mitandao ya jamii | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Waziri Ummy Mwalimu awataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuacha kuendekeza mitandao ya jamii



Na Ezekiel Mtonyole, Dodoma.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, amewataka maafisa Maendeleo ya Jamii hapa nchini kuacha kupoteza muda katika mitandao ya kijamii, kutumiana vichekesho, badala yake watumie mda huo kupeana elimu ya Afya.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Maafisa Maendeleo nchini uliofanyika katika jiji la Dodoma.

Amesema sasa hivi teknolojia inatumika vibaya kwa kuingia kwenye WhatsApp na maeneo mengine kwa kutumiana vikatuni visivyo na maana badala ya kujifunza kuhusu Kilimo,ufugaji,elimu ya afya ambavyo vina manufaa kwa jamii.

"Naomba tumieni simu katika kurahisisha utendaji wenu kama mimi hivi sasa kazi nyingi nazifanya kupitia simu na sio kuchati vitu vya ajabu ajabu wakati Kuna Mambo ya msingi ya kufanya," amesema Waziri Ummy.

Aidha  amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kujenga umataduni wa kwenda kufuata takwimu za ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto na mimba za utotoni kwa jeshi la polisi badala ya kusubiri takwimu za jeshi la polisi.

Ameongeza kwa kusema "naomba mjenge utaratibu wa kuwa na takwimu ofisini kwenu na kuzitumia,nimeshawahi kwenda mikoani kazi ya Maendeleo ya jamii lakini napokelewa Mganga Mkuu wa mkoa  na wilaya lakini maafisa maendeleo wanatoweka kitendo ambacho mnajirudisha nyuma nyie wenyewe," amesema Ummy.

Kuhusu takwimu Waziri amesema asilimia 37 watoto wamebakwa,huku asilimia 27 ikiwa ni ndoa za utotoni wakati asilimia 10 ni ukeketaji ambavyo vyote vinapingwa vikali na serikali.

Amesema kwa takwimu hizo inaonyesha kuwa  jinsi gani wananchi wamepata uwelewa juu ya utoaji taarifa wa ukatili unaofanywa na jamii katika maeneo mbalimbali hapa nchini amewataka  maafisa Maendeleo ya jamii kuchangamka kuanzia sasa ili kuweza kupata takwimu zaidi za vitendo hivyo katika maeneo mbalimbali.

Aidha ametumia mda huo kuzindua mwongozo wa majukumu ya wataalamu wa maendeleo ya jamii katika sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa ambazo zitawasaidia katika utendaji kazi wao.

Mbali na mwongozo huo pia amekizindua rasmi Chama cha maafisa Maendeleo nchini (CODEPATA)

Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Maendeleo ya jamii Nchini Patrick Golwike amesema katika mkutano huo kutakuwa na mada 10 za kuleta Maendeleo ambazo zitajadiliwa kupelekea kuhitimisha kwamkutano huo wa mwaka.