Viwanja vya Ndege Tanzania kutumika majira yote ya mwaka

Viwanja vya Ndege Tanzania sasa vinaweza kutumika majira yote ya mwaka ya masika na kiangazi kutokana vingi barabara zake za kutua na kuruka ndege kujengwa kwa kiwango cha lami, imeelezwa.

Mkurugenzi wa Idara ya Uhandisi na Huduma za Ufundi, Mhandisi Mbila Mdemu ametoa maelezo hayo leo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), alipozungumza na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, wakati alipozungumzia mafanikio ya Mamlaka hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Mhandisi Mdemu amesema Mamlaka inajivunia mafanikio ya kuwa na viwanja 16 vyenye barabara za kutua na kuruka ndege za kiwango cha lami, ambazo zinaruhusu kutumika kwa kipindi chote cha mwaka bila matatizo ya aina yeyote.

Viwanja hivyo ni Arusha, Tabora, Mwanza, Bukoba, Mafia, Iringa, Songwe, Tanga, Moshi, Songwe, Kigoma, Dodoma, Mtwara, Mpanda pamoja Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA).

“Tangu kuanzishwa Mamlaka vilikuwepo viwanja nane pekee vyenye viwango vya lami, lakini sasa mpaka Novemba mwaka 2015 tumeweza kuongeza na kufikisha 16 ambavyo vinapitika kwa uhakika zaidi katika majira yote ya mwaka ya kiangazi na masika,” amesema Mhandisi Mdemu.

Mbali na barabara za kutua na kuruka ndege, pia Mamlaka hiyo imefanikiwa kufanya ukarabati na upanuzi wa majengo ya abiria na kufanikisha kuweza kuhudumia abiria wengi zaidi ya wa awali, ambapo ni pamoja na jengo la tatu la abiria la JNIA, Bukoba, Dodoma, Iringa, Mpanda, Mtwara na Mwanza.

Pia Mhandisi Mdemu amesema mafanikio mengine ni kuboresha ulinzi wa kutosha wa abiria na mizigo, kwa kufungwa kamera za kufuatilia matukio, kuwepo kwa mashine za kukagua abiria na mizigo na kujengwa kwa uzio kwenye baadhi ya viwanja,; pia kumefungwa mifumo ya kisasa ya kiyoyozi; na kuanza kusimikwa kwa taa za kuongoza ndege ili ziweze kutua usiku.

Naye Meneja Mipango na Takwimu wa TAA, Asteria Mushi amesema kuwa Mamlaka imeweza kupata mafanikio kwa kuongeza mapato kutoka Tshs. Bil. 63 kwa mwaka 2015 na kufikia Bil. 105 kwa mwaka 2018, ambazo ni ongezeko la asilimia 66, ambapo lengo la Mamlaka ni kuongeza mapato na kufikia Tshs. Bil. 130 ifikapo mwaka 2020; pia wameweza kuongeza biashara za maduka na sasa serikali wanashirikiana na taasisi binafsi kujenga hoteli ya nyota nne yenye ghorofa nane (8) itakayojengwa karibu na jengo la pili la abiria (JNIA-TBII).

Hali kadhalika Mushi, amesema Mamlaka imeongeza idadi ya ndege za abiria ambazo awali zilikuwa zikifanya safari nchini, lakini baadaye zikasitisha na zimeanza tena safari hizo, ambazo ni Air Uganda na Zimbabwe. Ndege hizo zinafanya idadi ya ndege za nje kufikia 21.

“Katika viwanja vya ndege tumetenga asilimia 30 kwenye majengo ya abiria tumetenga huduma za abiria na biashara, lakini tunaangalia na ongezeko la ndege za Air Tanzania ambapo sasa zinakwenda njia 10 za ndani ya nchi na njia tano za kimataifa,” amesema Mushi.