Na John Walter, Babati.
Shule ya Msingi shikizi ya Maweni (Malesh) iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoani Manyara yenye wanafunzi 242, ina Mwalimu mmoja tu licha ya kuwa na madarasa manne na hivyo kumfanya ashindwe kuwamudu wanafunzi ipasavyo.
Hayo yalibainishwa na Mwalimu wa mkuu wa shule hiyo Jacob Mwenda wakati akizungumza na kamati ya siasa ya wilaya ya Babati na wananchi.
Mwalimu Mwenda alisema shule hiyo ina madarasa kuanzia awali hadi darasa la tatu huku akidai masomo yote ndio anayafundusha.
Alisema darasa moja anaweza kufundisha masomo mawili ili kila mwanafunzi aweze kuambulia kitu.
"Naiomba serikali inisaidie kuongeza walimu angalau walimu tuwe wanne ili tuweze kufundisha wanafunzi hawa,"Alisema Mwalimu Mwenda
Katibu wa chama Cha mapinduzi(CCM) Filbert Mpwepwe aliwataka viongozi wa Kijiji cha Endadosh na kata ya Qash kuongeza jitihada ili shule hiyo ikamilike haraka.
Alitumia fursa hiyo kuwataka kuongeza idadi ya mafundi ili kazi iende haraka.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Babati Nicodemus Tarmo alisema shida iliyopo wanachi wa Kijiji hicho hawajitumi licha ya Halmashauri kuwachangia sh. Milioni tano.
Tarimo alisema ili shule iweze kupata usajili ni lazima iwe imekamilisha ujenzi wa miundo mbinu kwa asilimia 75.
Alimtaka diwani wa kata hiyo kuwachukulia hatua wenyeviti wa vitongoji wanaokula fedha ya michango ya wananchi na siyo kulalamika.
Diwani wa kata ya Qash John Kanda alisema kitu kinachokwamisha ujenzi wa shule hiyo ni wenyeviti kukusanya fedha na kuzitafuna pamoja na watendaji wavijiji.
Naye Rukia Kemo alisema kwa hali iliyopo shuleni hapo ya kuwa na Mwalimu mmoja uwezekano wa watoto kufanya vizuri ni mgumu kama serikali haitawapelekea walimu.
Aliongeza kuwa wanahitaji watoto wao wafaulu ila kukosekana kwa walimu kunawapa mashaka sana