Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ametoa pikipiki 448 kwa maafisa Tarafa wote hapa nchini ambapo, Mkoa wa Dodoma wenye tarafa 28 umepata mgao wa pikipiki 28 kwa ajili ya Maafisa Tarafa wote wa Mkoa huo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge, akikabidhi pikipiki hizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Patrobas Katambi kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya wote wa Mkoa wa Dodoma ili wazikabidhi kwa Maafisa Tarafa Mkoani humo, amewatahadharisha Maafisa Tarafa wote Mkoani Dodoma watakaopewa pikipiki hizo, kutothubutu kuzitumia pikipiki hizo kwa kuzifanyia biashara ya Bodaboda.
Dkt. Mahenge amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma Gilles Muroto, kuwaelekeza Wakuu wa Polisi wa Wilaya zote za Mkoa wa Dodoma, kuhakikisha wanawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria Maafisa Tarafa wote watakao zitumia pikipiki hizo za Serikali kwa kufanyia biashara binafsi kama bodaboda badala ya kuzitumia kuwafikia wananchi kwenye maeneo yote ya Tarafa zao kusimamia utoaji huduma za kijamii, kiuchumi na kiutawala.
“Maelekezo yangu kwenu, hizi ni pikipiki za kazi za Serikali, sio pikipiki za bodaboda, matokeo yake, tunatarajia kuona Maafisa Tarafa mnafika kwenye maeneo yenu yote na kuwa mnawasilisha taarifa ya kazi mbalimbali kwenye maeneo yenu” aliongeza Dkt. Mahenge.
Alitumia hafla hiyo kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwa, katika kipindi cha uongozi wake amefanya mengi kwenye sekta za Afya, Miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na sekta ya anga, reli, usafiri wa majini, nishati, madini, elimu, ukusanyaji mapato na sasa katika kuboresha utendaji wa serikali, ameimarisha utendaji wa Maafisa Tarafa ambao ni kiungo muhimu kwa kuwawezesha usafiri wa pikipiki.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Ndg. Maduka Kessy amesema Mkoa wa Dodoma una jumla ya Tarafa 28 na Mhe. Rais Magufuli amewapatia pikipiki Maafisa Tarafa wote wa Mkoa huo na kuwa jambo hili linaimarisha uwezo wa Maafisa Tarafa kuwafikia wananchi wote kwenye maeneo yao ya Tarafa na pia ufanisi katika kusimamia shughuli za serikali.
Akipokea Pikipiki hizo kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Patrobas Katambi amesema kuwa changamoto kubwa iliyokuwa inawakabili Maafisa Tarafa katika kusimamia na kutekeleza shughuli za Serikali kwenye ngazi za Tarafa ilikuwa ni ukosefu wa Usafiri na sasa Rais Magufuli ametatua changamoto hiyo kwa nchi nzima. Aidha, amewataka Maafisa Tarafa kwenda kuzitunza pikipiki hizo.
Akishukuru kwa niaba ya Maafisa Tarafa wote Mkoani Dodoma, Lucas Mbise Afisa Tarafa ya Zuzu Jijini Dodoma, amesema pikipiki hizo ni ahadi ya Mhe. Rais Magufuli aliyoitoa Juni 4, 2019 alipokutana na Maafisa Tarafa hao Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuahidi kuwapatia pikipiki kutokana na mazingira ya maeneo yao ya kazi ili kuwaongezea ufanisi.