Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amemkosoa vikali waziri wa fedha Tito Mboweni kuhusu matamshi aliyoyatowa kupitia mtandao wa kijamii juu ya kuondolewa kwa gavana wa benki kuu ya Zambia.
Tangazo hilo limetolewa leo na ofisi ya rais huyo wa Afrika kusini. Rais wa Zambia Edgar Lungu alimtimua gavana wa benki kuu ya nchi yake Denny Kalyalya siku ya Jumamosi bila ya kutowa maelezo.
Waziri wa fedha wa Afrika Kusini Mboweni ambaye aliwahi kuwa gavana wa benki ya akiba ya Afrika Kusini kupitia ujumbe wake wa Twitta ambao umeshafutwa kwenye ukurasa wake alimtaka rais Lungu atowe ufafanuzi wa hatua yake hiyo.
Kimsingi sio hali ya kawaida kwa maafisa katika nchi nyingine kutoa kauli za kuzungumzia wazi kuhusu hatua ya uteuzi na kufutwa inayofanyika katika nchi nyingine.
Katika mojawapo ya ujumbe waziri Mboweni ametowa ahadi ya kuchukua hatua ikiwa sababu hazitotolewa kwanini gavana huyo wa benki kuu ya Zambia amefutwa kazi na rais Lungu.
Rais wa Afrika Kusini Ramaphosa kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake ameihakikishia serikali na wananchi wa Jamhuri ya Zambia kwamba kauli hiyo ya kusikitisha ya waziri wake wa fedha haiwakilishi msimamo wa Afrika Kusini.
0 Comments