KwA kawaida mwanaume ana korodani mbili ambazo zimehifadhiwa katika mfuko maalum wenye tabaka tatu na ndani kuna kiasi kidogo cha maji kinachozunguka korodani ili kuilinda. Mwanaume endapo atakuwa na korodani moja ni tatizo na pia akiwa hana kabisa korodani ni tatizo kubwa.
Kazi ya korodani ni kuzalisha mbegu za kiume, mwanaume anaweza kuwa na korodani zote mbili lakini akashindwa kuzalisha mbegu za uzazi kutokana na matatizo mbalimbali.
Mwanaume mwenye korodani moja anaweza kuzalisha mbegu au asizalishe kabisa, kitu cha msingi akapimwe hospitali kuona uwezo wa hiyo moja. Mwanaume ambaye hana korodani kabisa hawezi kuzalisha mbegu za uzazi hivyo hana uwezo wa kumpa mimba mwanamke. Tatizo la kuwa na korodani moja au kukosa kabisa tutakuja kuliona katika makala zijazo.
Jinsi tatizo linavyotokea
Maumivu ya korodani hutokea katika korodani au haswa moja au zote mbili endapo zitaumizwa kwa kuumia au maambukizi. Maambukizi haya yanaweza kuwa makali na ya muda mfupi,yanakuwa makali kwa muda fulani halafu yanapoa yenyewe au kwa dawa baadaye yanarudi tena yakiwa makali sana kama mwanzo au pia huwa sugu yaani unakuwa na maumivu ambayo siyo makali ila ni ya muda mrefu na yanayokunyima raha.
Maumivu ya korodani yanaweza kuwa makali kiasi kwamba yatahitajika matibabu ya dharura mfano korodani inavimba kama jipu kubwa, ikiambatana na maumivu makali na homa, tatizo hili kitaalam huitwa ‘Fournier's gangrene' au inatamkwa ‘Fonias gangrini'.
Vilevile inaweza kutokea korodani ikajinyonga yenyewe na kusababisha ukapata maumivu makali ya ghafla yanayoelekea hadi tumboni, tatizo hili linaitwa Testicular Torsion.
Chanzo cha tatizo
Maumivu ya korodani yana vyanzo mbalimbali, lakini maumivu sugu ni yale yanayochukua takriban zaidi ya miezi mitatu. Maumivu makali na ya ghafla huwa hayavumiliki na huwa na tiba ya dharura. Maumivu haya sugu huwa kwa kipindi fulani hasa kwa wanaume ambao wametoka kufunga uzazi Vesectomy lakini baadaye hupoa. Vilevile husababishwa na maambukizi katika korodani na kusababisha magonjwa kama Epididymits, Prostatis na Orchitis ambayo yote ni maradhi ya viungo vya uzazi vya mwanaume na husababisha ugumba.
Vilevile korodani inaweza kuwa na vivimbe kwa ndani, pembeni au juu ya kokwa au kuizunguka. Uvimbe au vivimbe hivi vinaweza kuwa na mishipa ya damu iliyojikunja humo, kujaa maji isivyo kawaida, mbegu za kiume kujikusanya na kushindwa kutoka na mengine ya kitaalam ambayo pia tutakuja kuyaona.
Yote haya humsababishia mwanaume ugumba. Maumivu pia husababishwa na kuumia korodani au baada ya kufanyiwa upasuaji kama tulivyokwishaona hapo awali.
Maumivu yatokanayo na korodani au kende kujinyonga huwa makali sana na korodani zikiguswa huuma sana na kawaida huendelea hivyo kwa masaa yasiyozidi sita.
Unapoona dalili kama hizo wahi kamuone daktari kwa ajiri ya uchunguzi zaidi.
Kwa kawaida maumivu ya korodani hupanda juu zaidi na kuacha mfuko wake mtupu. Tatizo hili huwatokea zaidi vijana chini ya umri wa miaka 25 ingawa pia inaweza kutokea katika umri zaidi ya huo.
Tatizo hili huhitaji upasuaji wa dharura.
Wakati mwingine tatizo hili hutokea kwa korodani kuwa na tabia ya kupanda au kushuka, ikishuka mgonjwa hupata nafuu, hali huendelea vivyohivyo kwa vipindi fulani. Hali hii inapotokea mgonjwa hutapika na kukosa nguvu.
Maambuziki ya korodani pia mtakuja kuyaona kwa undani baadaye lakini pia huambatana na maambukizi katika mkojo au ‘UTI' na homa. Huwa makali kwa vipindi. Kisonono na gono huchangia tatizo hili kwa kiasi kikubwa.
Uvimbe kama jipu wa korodani au Fonias gangrini kama tulivyoona hapo awali ni mbaya kwani korodani inakuwa kama inaoza halafu tatizo hilo lina tabia ya kusambaa kuelekea uvunguni jirani na njia ya haja kubwa. Uvimbe huwa kama busha au jipu kubwa lakini ndani yake hakuna maji wala usaha.
Tatizo hili pia tutakuja kuliona kwa undani kwani nalo huathiri wanaume wengi na ni tatizo kubwa ambalo mwanaume yeyote ni rahisi kupata pia hupoteza uwezo wa kuzaa.
Korodani kushindwa kufanya kazi (test cular failure)
Kazi ya korodani ni kuzalisha vichocheo au homoni za kiume na mbegu za kiume. Mwanaume anatakiwa awe na korodan mbili ingawa ukiwa na moja pia inaweza kufanya kazi kama ni nzima, inatakiwa kama unayo moja nenda hospitali ukapimwe kuthibitisha ubora wake na uwezo wake.
Katika hali isiyo ya kawaida wapo wanaume wenye korodani tatu. Ukishakuwa na hali hii ni vema ukapimwe hospitali.
Matatizo mengi ya korodani tumeshayaona kwa kina katika matoleo yaliyopita na tunamalizia kuyaona leo huku tukiangalia na mada hii.
Matatizo ya korodani kama tulivyoyaona ndiyo matokeo ya kushindwa kufaya kazi. Korodani kushindwa kufanya kazi tunaweza kuweka katika makundi mawili, kwanza ni hali ya uwezo wake kuwa mdogo tangu balehe Hypogonadism' na tatizo linaweza kutokea ukubwani yaani baada ya balehe au utu uzima secondary hyponadism.
Tatizo linapotokea katika utu uzima huambatana na upungufu wa nguvu za kiume, kusinyaa korodani na uume kuwa mfupi au mdogo.
Hii ni kutokana na korodani kushindwa kuzalisha vichocheo au homoni za kiume kama tatizo ni tangu balehe, basi hali ya matatizo makubwa hutokea katika mfumo wa uzazi na mwili kwa ujumla. Hayo ni baadhi tu ya matatizo ila mengi tutaendelea kuyaona.
Chanzo cha tatizo
Korodani kushindwa kufanya kazi husababishwa na matatizo mengi kama vile matumizi ya madawa baadhi yake ya hospitali kwa muda mrefu hasa kwa wanaume mfano dawa za jamii ya Glucocorticoids, Ketoconazole, na madawa ya kulevya hasa bangi.
Matatizo ya kuzaliwa nayo Chromosome Problems magonjwa yanayoathiri korodani mfano Mumps na joto kali na la muda mrefu katika korodan. Kuumia moja kwa moja kwa korodani Direct Injury na kuvimba na kujinyonga kwa korodani Testicular Torsion.
Watu ambao wapo katika hatari kubwa korodani zao kuja kushindwa kufanya kazi ni wale ambao hufanya shughuli zinazoumiza korodani zao taratibu na kwa muda mrefu mfano waendesha pikipiki au bodaboda katika barabara mbovu kwa muda mrefu, huwa kitaalamu huziumiza korodani zao Constant low level injury to the Scrotum na wale ambao wana korodani moja au hawana kabisa.
Dalili za tatizo
Endapo korodani zako zinashindwa kuzalisha mbegu za kiume utajikuta unaishi na mke kwa zaidi ya mwaka mmoja na mnafanya tendo la ndoa kwa lengo la kutafuta mtoto na mnakosa.
Endapo korodani zinashindwa kuzalisha homoni za kiume basi utakuwa na dalili zifuatazo, kama ni mtoto anakuwa harefuki anaendelea kuwa mfupi huku umri unaenda, matiti ya mtoto wa kiume au kijana yanakuwa makubwa Gynecomastia mwili hauwi na misuli imara, kukosa hamu ya tendo la ndoa, unakuta vinyweleo vya kwapani na sehemu za siri havioti au kama vilishaanza kuota havikui hata kwa zaidi ya mwaka, huoti ndevu na kubadilika kama mwanaume, uume haukui na korodani zinasinyaa na kuwa kama za mtoto. Sauti haiwi nzito.
Uchunguzi
Matatizo ya viungo vya uzazi huchunguzwa katika hospitali za wilaya na mkoa, uchunguzi wa awali hufanyika kwenye vituo vya afya.Vipimo mbalimbali hufanyika kadiri daktari atakavyoona inafaa.
Ushauri
Matibabu huchukua muda mrefu baada ya uchunguzi wa kina. Matibabu ya dharura hufanyika pale kunapokuwa na maumivu makali. Ni vema kuepuka maambukizi hasa ya magonjwa ya zinaa na kuwahi hospitali pale unapohisi una tatizo.
0 Comments