F Mpango wa mazoezi wa kupunguza tumbo kwa mama aliyetoka kujifungua | Muungwana BLOG
https://c2p.cleverwebserver.com/dashboard/6a0bec4b-79ba-11ef-ad2b-06f0639468d1

Mpango wa mazoezi wa kupunguza tumbo kwa mama aliyetoka kujifungua

 

Suala la kupunguza tumbo ama uzito mara baada ya kupata operesheni ya uzazi, limekuwa ni changamoto miongoni mwa wanawake wengi.

Wengi wamekuwa wakishindwa kurudisha maumbo yao ya awali mara watokapo kujifungua. Hii inatokana si tu kushindwa kupangilio milo yao kwa kuchagua vyakula vyenye afya, bali pia na kushindwa kufanya mazoezi kwa ajili ya kujenga miili yao.

Kama ilivyo kwa wazazi wengine huwa na uchu wa kurudisha miili yao haraka iwezekanavyo, na muda mwingine kupangilia vyakula maalumu vyenye afya vitakavyokuongoza kufikia malengo yako hakikisha unakuwa na programu maalumu ya mazoezi salama itakayokurahisishia zaidi lengo lako hilo.

Kabla ya kuanza mpango wako huo wa kuboresha umbo lako, kumbuka kwamba mwili wako umetoka katika utaratibu mwingine wa kumleta kiumbe duniani tena kwa njia ya upasuaji. Hivyo suala la kupungua kwako au kurudi kwako katika hali ya kawaida linatakiwa liende taratibu ili kutoathiri afya yako. Kamwe usijifananishe na yule aliyejifungua kwa njia ya kawaida.

Kama umetoka katika operesheni ya uzazi, ni wazi kuwa utakuwa na kovu. Ni muhimu sana kukinga kovu hilo na kulipa muda lipone taratibu.

Ni vyema ungeanza mpango wa kupunguza uzito ama tumbo lako mara baada ya kupata ushauri wa daktari. Yeye ndiye mwenye mamlaka ya kukuruhusu kuanza, hasa baada ya kurudhika na maendeleo ya afya yako.

Madaktari wengi wamekuwa wakiwashauri wanawake kusubiri hadi wiki sita hadi nane kabla ya kuanza mazoezi rahisi yatakayokuwa na lengo la kupunguza uzito yakiambatana na ale ya kupunguza tumbo.

Kukinga kovu lako
Ni kweli kabisa wanawake wengi wamekuwa wakipenda kuvaa suruali maalumu ili kuficha kovu katika tumbo, lakini pia wengine hufanya hivyo wakilenga kuficha hata tumbo lenyewe ambalo limetokea kukua visivyo kawaida baada ya operesheni. Hii ni sawa. Lakini pia unashauriwa kupata ushauri wa daktari kabla ya kuamua kuvaa hivyo.

Mazoezi.
Ikiwa wewe ni mmoja kati ya wanawake waliofanyiwa operesheni na unazingatia kula vyakula bora na kufanya mazoezi sahihi tayari utakuwa uko kwenye njia sahihi ya siyo tu kupunguza uzito wa mwili, bali pia ukubwa wa tumbo lako.
Mazoezi ya viungo kama vile kukimbia, kuogelea, kutembea hata kuendesha baiskeli yatakusaidia kuunguza mafuta na pia kupunguza uzito.

Unaweza pia kuanza kufanya mazoezi madogo madogo ya tumbo kwa kulala na kunyoosha na kukunja misuli yako ya tumbo. Misuli yako itakapokuwa imejengeka unaweza kuanza mazoezi ya ‘sit-ups’.

Ikiwa utaamua kufanya mazoezi kwenye darasa maalumu au hata gym hakikisha unamweleza mwalimu wako kuwa umefanyiwa operesheni hivyo itakuwa rahisi kwake kukupa mazoezi yanayoendana na hali yako.

Kwa upande wa chakula, kila mara unatakiwa kuwa karibu na daktari wako ili uende katika mstari sahihi katika huo ulaji wako. Yeye anaweza akakushauri ni chakula gani ule na kipi uache.

Mazoezi yafanye kwa muda gani
Kutokana na utofauti tulionao mara nyingi kila mmoja inamchukua muda wake kupunguza ukubwa wa tumbo ama uzito wa mwili wake.

Mwanamke aliyewahi kuzaa mara nyingi anahitaji kazi ya ziada ukilinganisha na yule anayezaa kwa mara ya kwanza. Pia wanawake wembamba wana uwezo wa kufanya vizuri zaidi kuliko wale wanene.

Si vyema kujilinganisha na mtu katika mpangilio wako huu wa mazoezi, kwani wakati mwingine unaweza ukajilinganisha na mtu ambaye si sahihi kwako.

Unachotakiwa kufanya ni kuelekeza nguvu zako katika kufanikisha lengo lako.

Post a Comment

0 Comments