Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo,ametembelea na kukagua utendaji kazi wa miradi mikubwa ya kimkakati katika jiji la Dodoma ikiwa ni Soko ya Ndugai, Kituo kikuu cha mabasi, na sehemu ya maegesho ya malori Nala na kutoridhishwa na utendaji kazi kwa baadhi ya maeneo.
Huku akitoa siku 12 kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuhakikisha inarekebisha dosari alizoziona katika miradi hiyo ili ifanyekazi kwa ufasaha kama ilivyokusudiwa.
Waziri Jafo amesema amebaini baadhi ya maeneo katika soko la Ndugai bado hayana wafanyabiashara huku kukiwa na mwamko mdogo wa ufanyaji biashara kwenye eneo hilo.
Amesema Serikali imetumia fedha nyingi katika kujenga miondombinu hiyo ya mabilioni ya fedha kwa ajili ya wananchi lakini ufanisi wake bado hauonekani na kutaka kuwekwa mikakati zaidi kuongeza mwamko na mzunguko wa biashara maeneo hayo.
“Yaani kutokana hapa hadi mjini kati ni umbali wa kilomita nane, inashangaza kuona mradi huu ambao umekamilika kwa muda mrefu wa soko lakini mwamko wa biashara hakuna na maeneo mengine bado hakuna wafanyabiashara, hii kwa kweli haijaniridhisha,”amesema Mhe. Jafo.
Ameongeza kuwa “Hili eneo la soko bado lipo wazi mmeshindwa nini siku zote kufanya? Nataka soko hili liwe ‘busy’, haiwezekani muwekewe miradi mikubwa ya gharama kubwa halafu haina watu, sijaridhishwa kabisa na hili soko hakuna kinachofanyika
“Kodi zinazotozwa ziwe rafiki kwa wananchi maana hii miradi ni kwa ajili yao, soko hili limejengwa kwa fedha za serikali na si za mkopo hivyo msiwatoze fedha kubwa kama vile mnarejesha mkopo benki,”amesema.
Akiwa katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo Mikoani, Waziri Jafo ameiagiza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuhakikisha wanashughulikia kero zilizopo kwenye kituo hicho ili kifanye kazi kwa ufanisi kama kilivyotarajiwa.
“Kuna malalamiko kuhusu mageti na abiria kutembea umbali mrefu kutoka ndani hadi kwenye kituo cha daladala, na mengine kidogo naagiza yashughulikiwe ili hawa wafanyabiashara wasipate kikwazo,”amesema.
Ameongeza kuwa “Uwekwe uhuru wa kuingia humu, pia hawa mawakala wa mabasi na wapiga debe wapewe vitambulisho ambavyo watavilipia na kurahisisha utendaji kazi wao na kuongeza mapato,”amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Joseph Mafuru, amemuahidi Waziri kwamba atashughulikia maelekezo yote huku akibainisha kuwa katika soko ndani ya wiki mbili kunatarajia kuwekwa gulio na shughuli zingine za kiuchumi jambo ambalo litaongeza mzunguko wa biashara kwenye eneo hilo.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt.Binilith Mahenge amesema uongozi wa Mkoa utahakikisha shughuli za kibiashara kwenye maeneo hayo zinachangamka na hatua mbalimbali zimechukuliwa ili kuleta ufanisi zaidi katika miradi hiyo iliyoigharimu fedha nyingi Serikali hadi kukamilika kwake.
0 Comments