Na John Walter -Babati
Katika kuadhimisha Sikukuu ya Eid Ul-Fitr, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa mkono wa kheri kwa wazee na watoto wenye uhitaji kwa kuwapatia sadaka ya vyakula na mahitaji mengine muhimu.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, alikabidhi sadaka hiyo Machi 30, 2025, katika Kituo cha Ustawi wa Jamii Sarame Magugu kwa wazee na kwenye vituo vya watoto wenye uhitaji vya Zilper Foundation, Hossana Home Care Foundation, na Manyara Holistic Center, vilivyopo Wilaya ya Babati.
Akiwasilisha sadaka hiyo, Mhe. Sendiga amesema Rais Dkt. Samia ana desturi ya kushiriki sikukuu na makundi yenye uhitaji kwa kuwapatia msaada wa vyakula na mahitaji mengine ili waweze kusherehekea kwa furaha.
"Leo tumekabidhi mchele, sukari, mafuta ya kula, mafuta ya kujipaka, sabuni, vinywaji, chumvi, miswaki, dawa za meno, na mbuzi kwa ajili ya kitoweo ili wazee na watoto hawa washerehekee Eid kwa amani na furaha," alisema Sendiga.
Viongozi wa vituo vilivyonufaika na msaada huo, wakiwemo Neema Munis, Mkurugenzi wa Kituo cha Hossana, na Maige Kigendi, Afisa Ustawi wa Kituo cha Wazee Sarame, waliishukuru serikali kwa kutambua na kuthamini makundi hayo maalum.
Sadaka hiyo ya Rais Dkt. Samia imeleta faraja kwa wazee na watoto hao, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha makundi yote yanashiriki kikamilifu katika furaha ya sikukuu za Eid na Pasaka.
0 Comments